1 Nikimwona napata wazimu, Siniwate nitenda kuzimu
Nataka nimchonge sanamu, Dunia yote naifahamu
Ilahi aniwekee wewe
2 Nilimuona huko awali, Yakanijaa mengi maswali
Mrembo atakosa rijali, 'Kajipa moyo bila kujali
Nikasema langu pendo
3 Anajua vyema kujipamba, Avae gunia anabamba
Mchezoni ni Pele wa samba, Kwayo mapenzi yake natamba
Kashaniroga na huba
4 Mwili wavutia macho yangu, Haishi hamu samaki changu
Kumuoa kusudio langu, Chakwangu chake chakwake changu
Nampa mwili mzima
5 Miye ndege nae ni kiota, Nikilala ndie namuota
Nitamganda sitamuwata, Kila mahali kanikamata
Abadi sitamgua
✍🏿Abuuabdillah