بسم الله الرحمن الرحيم
SHAIRI:-
KUTAHADHARI NA IDI ZA MAKAFIRI.
1- Nainyanyua kalamu, ujumbe uweze fika,
Sifa njema kwa Qayumu, asiyenamshirika,
aloiweka nidhamu, dini ilotakasika,
dini yetu isilamu, kinyume kukhasirika.
2- Alomuumba Adamu, umbile lakusifika,
bila baba wala 'Hamu’ wala mama kadhalika,
kisha kwa tone la damu, wengine wakafurika,
Ewe Mola Muqadimu, kwa mema unasifika.
3- Husifiki na kuzaa, kuzaliwa kadhalika,
unachotaka ni twaa, ibada zako kushika,
mwisho pepo au laa, motoni kuadhibika,
Jitahadhari kukaa, na waliofilisika.
4- Walioiacha njia, shiriki wakajivika,
wakaabudu nabia, umwana wakamtwika,
na sanamu la bandia, kutani wakabandika,
naye ni kiumbe pia, na kifo kitamfika!
5- Naye ni mja kiumbe, matatizo humfika,
fadhila yake ujumbe, muongozo kumulika,
akataze chembechembe, yote yasohitajika,
kwa watu wake wapambe, si dunia Afirika.
6- Chunga na zao sherehe, pamoja kufurahika,
wakikuita samehe, usende ukaitika,
kufuru usiendee, Mtoto wake Rabuka!
Sifa njema za pekee, Karima alotukuka.
7- Epuka yao mavazi, na vyote wanavyopika,
umpwekeshe Azizi, mbali nao kujiweka,
usifanyie ajizi, jambo zito si kucheka,
hana mtoto Mjuzi, ni uzushi wameweka.
8- Iheshimu yako dini, chunga na yake mipaka,
hasahasa waumini, Kirisimasi Pasaka,
usighuri ujirani, mualiko ukadaka,
utamuudhi Manani, kwa madai mpya mwaka!
9- Watoto tuwazuie, hata ndani kuwaweka,
kwenye hili wafungie, wasije nje kucheka,
hovyohovyo wajilie, watajakula vibweka,
kwa uwazi waambie, Diniyo haki tosheka.
10- Nasaha zisambazeni, nje ya nchi mipaka,
nduguzo elewesheni, madada hadi makaka,
kwa Mola kesho mbeleni, na safu za malaika,
Naifunga yangu peni, na tamati nimefika.
_______
✍🏽 Abuu Maysarah' Saalim bin Ramadhaan.
Jumamosi 30- Jumaadal Uwlaa- 1444 H.
24-12-2022 M.
Na Allah ndio mjuzi.